Bati 96 (gauge 28) zenye thamani ya Tsh 3,270,000/- zimekabidhiwa Shule ya Msingi Rubya kwa ajili ya kuezeka madarasa mawili ambayo yatajengwa na jamii inayozunguka eneo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Kan. Denis Mwila ambaye ni Mgeni Rasmi katika tukio hilo la makabidhiano, amewashukuru Wakala wa Misitu Wilayani hapa chini ya Shamba la Miti Rubya kwa Kutoa bati hizo ambazo zitatumika kwa maslahi mapana ya kuboresha miundombinu ya Shule ya msingi Rubya.
Pia amewashukuru wananchi wote kwa kuendelea kulinda Misitu yetu kwani kwa Misitu itatusaidia kukabiliana na mabadiliko ya Tabia ya nchi, pia inatuletea mapato yanayotokana na mazao yake kama Mbao na ajira.
Mwila ametoa Rai kwa wananchi wa kata ya Bwiro na Muriti hasa kijiji cha Selema na wengine watakao guswa kuchangia uboreshaji wa miundombinu ya Shule hiyo kufanya hivyo kwani Shule hiyo bado ina hali mbaya.
“Bila kupepesa macho hali ya elimu katika Shule hii ni mbaya, wazazi tujitoe kuboresha miundombinu ya kusomea watoto wetu” Alisema Mwila.
Amesisitiza Shule hiyo inahitaji madarasa, madawati na kuongeza matundu ya vyoo.
Aidha Mwila ametoa wito kwa wakala wa Misitu TFS kupitia shamba hilo la miti Rubya kuendelea kuwa karibu na kuongeza nguvu katika kushirikiana na Shule.
Awali Festo N. Chaula Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Rubya ameeleza kuwa Shamba hilo wanashirikiana vema na jamii inayozunguka kwani imetenga jumla ya Tsh. 54,264,200/- kwa ajili ya ukarabati wa Zahanati ya Rubya inayohudumia wananchi na tayari tofali 2000 zimefyatuliwa, kwa mwaka 2021/22 wakala umetenga takribani milioni 54 kukarabati Kituo cha Polisi Rubya.
“Wakala unauhusiano mzuri na Halmashauri kwani ina ubia wa shamba la miti na pia inalipa ushuru wa Huduma kwa Halmashauri kutokana na mapato yake.” Alisema Chaula.
Meneja wa Wakala wa Misitu Wilaya ya Ukerewe Stephen O. Oyugi amesema Wakala utaendelea kushirikiana na jamii katika shughuli mbalimbali ambazo ni chachu ya Maendeleo na wataendelea na kutoa miche ya miti kwa jamii ambapo mpaka mwaka 2020/21 tumegawa miche 165,516 sawa na Tsh 49,654,800/-.
Mkwabi M. Mkunda Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Rubya ameshukuru wakala wa Misitu na shamba la miti rubya kwa msaada uliotoa ameahidi kusimamia bati hizo kufanya kazi kusudiwa kwa kushirikiana na jamii kujenga madarasa hayo.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.