Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ndg. John Mongella amefanya makabidhiano ya vitabu 38,891 vitakavyoenda kutumika katika shule za msingi kote wilayani ukerewe. Makabidhiano ya vitabu kwa Maafisa Elimu kata na Walimu wa kuu waliojitokeza katika eneo la kituo cha waalimu kujifunzia (TRC).
Afisa Elimu Msingi Reginald Richard akizungumza wakati wa makabidhiano hayo ameeleza Wilaya ya Ukerewe ina jumla ya Wanafunzi 108,812 wavulana wakiwa 54,820 na wasichana 53,992 kuanzia awali hadi darasa la saba. Wilaya ilikuwa na upungufu mkubwa wa vitabu hasa vya darasa la nne hadi kufikia uwiano wa kitabu kimoja kwa wanafunzi watano. Hali ya elimu inaenda inabadilika kutoka walipokuwa kwani mwaka 2017 walifaulu kwa 52.7% lakini kwa mwaka 2018 kwa matokeo ya Mock yaliyotoka mwezi huu mwanzoni wamepanda kwa 61.5%. “Baada ya kupokea vitabu hivi uwiano wa kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu ingawa lengo la serikali ni kufikia uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja” alisema Richard.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ndg. John Mongella amepongeza jitihada zinazoendelea kufanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe katika kunyanyua hali ya elimu katika wilaya ambayo inazidi kuboreka kadri siku zinavyokwenda. Amewataka walimu wa kuu kuendelea kusimamia vema walimu kutimiza wajibu wao vizuri na kuifanya wilaya upate ufaulu wa juu zaidi na kutumia vitabu hivyo kama nyenzo muhimu katika kufikia malengo ya elimu katika mkoa wa mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Ndg. Frank S. Bahati ameishukuru Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Elimu kwa kuendelea kuboresha hali ya elimu hasa katika Wilaya ya Ukerewe kwa kuleta vitabu 38,891 vitakavyoenda kuwa chachu ya ufaulu kwa wanafunzi na hivyo kunyanyua kiwango cha ufaulu. “Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea vitabu ilikupunguza tatizo la upungufu wa vitabu katika shule zetu za Msingi” alisema Bahati.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.