Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) Ukerewe kupitia mradi wa kunusuru kaya maskini umekamilisha zoezi la uhawilishaji fedha kwa dirisha la kipindi cha Machi - Aprili 2025 ambapo jumla ya kiasi cha shilingi milioni 362,517,000 kimetolewa kwa kaya 5,723 ndani ya Wilaya ya Ukerewe.
TASAF Ukerewe imekuwa na utaratibu wa kutoa elimu mbalimbali za msingi za kijamii kwa walengwa ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha wahusika wanaelewa matumizi bora ya kipato chao na kuimarisha mazingira ya maisha yao ya kila siku.
Aziz Makongo ni muwezeshaji kutoka TASAF Ukerewe amewataka walengwa wa TASAF wa kijiji cha Nkilizya kilichopo kata ya Nkilizya kujitathimini juu ya mafanikio waliyoyapata kwa kipindi chote cha mradi.
"..Ni wakati wa kutafakari kuhusu mafanikio hadi sasa ,kitu ambacho kitatusaidia kujua tulipotoka na tulipo.."
Maboga Bega ni mlengwa wa TASAF katika kijiji hicho cha Nkilizya yeye anasema mradi umemsaidia kukua kiakili kwa kuwa ameweza kukutana na wenzake wengi ambao wamekuwa wakiongea mara kwa mara nini wafanye angalau wakuze kipato chao na kujikwamua na umaskini uliokithiri.
"..Tumefanikiwa kuunda vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana,kwa kiasi flani mradi huu umenifundisha kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha,niseme tu TASAF ni mkombozi wa wanyonge.." amesema Maboga
Nae Mratibu wa TASAF Wilaya ya Ukerewe Bi.Jenitha Damaseni amewaweka wazi walengwa hao kuhusu ukomo wa mradi wa kunusuru kaya za walengwa (PSSN II) ifikapo Septemba 2025.
".. Tunataka kuhakikisha kuwa mpo tayari kuendelea na maisha hata baada ya mpango na kusherekea mafanikio mliyoyapata hata kama ni madogo angalau yameweza kukuvusha kutoka hatua moja hadi nyingine.."
Sophia Mataba ni mlengwa wa mpango huo katika kijiji cha Bukongo yeye anasema TASAF imemsaidia kujiimarisha kiuchumi.
"..Nilianza bila kitu baadae nikanunua mbuzi wawili baada ya mwaka wakaanza kuzaliana nikaanza kuuza kwa ajili ya kupata pesa ya matumizi ya nyumbani mpaka sasa nimebaki na mbuzi saba.Pia nina wajukuu wanne ambao wote wanahudumiwa na TASAF kiafya na kielimu.."
Akihitimisha zoezi hilo katika kijiji cha Nkilizya mwenyekiti wa kijiji hicho Alphaxard Pima amewaasa walengwa wote kufuata yote waliyofundishwa na kudumu katika vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana na kuimarisha upendo baina yao.
Uhawilishaji huo umefanyika kwa njia ya utoaji fedha taslim ambapo milioni 123,563,000 zimetolewa kwa walengwa 1,786 na kiasi cha shilingi milioni 248,954,000 kimewekwa kwenye akaunti na mitandao ya simu za walengwa 3,935.
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.