Serikali kupitia divisheni ya afya ,ustawi wa jamii na lishe wilayani Ukerewe imeendelea kuwajali wananchi wake kwa kufanya tathimini ya hali ya lishe na kutoa elimu katika maeneo mbalimbali ya minada na mikusanyiko ikiwa ni jitihada za kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na afya bora na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla .
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika mnanda wa Kakukuru uliopo kitongoji cha Makutano ndani ya kata ya Kakukuru Afisa lishe wa Wilaya ya Ukerewe ndugu Ditram Kutumile amesema lengo kuu la zoezi hilo ni kufanya upimaji wa hali ya lishe kwa watu wazima katika minada na mikusanyiko sambamba na kutoa elimu ya ulaji unaofaa na kubainisha jumla ya wananchi 500 wanatarajiwa kufikiwa ambapo hadi sasa watu 350 wamefikiwa sawa na 70% ya lengo.
Ditram ametoa elimu juu ya mtindo bora wa maisha huku akiwataka wananchi kuzingatia lishe bora yenye uwiano sahihi sambamba na kufanya mazoezi mepesi kama kutembea hali inayoweza kupunguza uwezekano wa kupata baadhi ya magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari,baadhi ya aina za saratani na shinikizo la damu.
Nae Afisa lishe katika hospitali ya Wilaya Nansio Bi.Julieth Peter amewaasa wananchi kuzingatia lishe bora inayofaa kwa kula makundi matano ya vyakula ambayo ni vyakula vya nafaka,jamii ya kunde,mbogamboga,matunda,mafuta na sukari bila kusahau maji kwa kuzingatia mchanganyiko wa kiasi unaofaa.
Ahadhi Mkaruka ni mwakilishi wa mwenyekiti wa kitongoji cha Makutano kilichopo kijiji cha Mulutirima anapongeza serikali kwa jitihada kubwa zinazoendelea za kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na elimu mbalimbali za afya huku akikiri huduma hiyo kuwa msaada mkubwa kwa watu kwa kuwaongezea ufahamu.
Revocatus Sebastian ni mkazi wa kisiwa cha Gana yeye amewashukuru wataalam waliotoa huduma hizo za afya huku akiomba ziendelee na zifike mbali zaidi hasa maeneo ya visiwa vingine vidogo vidogo vya Ukerewe.
Huduma nyingine zilizotolewa wakati wa zoezi hilo ni vipimo mbalimbali vya kiafya kama vile kupima uwaino wa uzito na urefu (BMI),hali ya lishe,kipimo cha presha na ushauri wa kiafya vilitolewa bure .
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.