Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania Lazaro Twange Upande wa Utekelezaji, akiwa na wataalamu wa mamlaka hiyo wamefanya ziara na kukabidhi madawati 185. Makabidhiano hayo yamefanyika katika shule ya msingi Nkilizya yaliyotolewa kusaidia jitihada za serikali ili kukabiliana na upungufu wa madawati katika shule za Msingi wilayani Ukerewe. Ambapo yatawasaidia wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa juu.
Lazaro Twange alieleza kuwa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania inasera ya kusaidiana na jamii kwenye jitihada zao za kujiletea maendeleo. Mamlaka ya Usimamizi Bandari Tanzania ni taasisi ya Umma ambayo kwa muongozo wa sasa wa serikali faida tunayoipata hua inatengwa kwa kazi na sehemu nyingine hutumika kusaidia wananchi katika jitihada za kujiletea maendeleo katika sekta mbalimbali kama elimu na afya.
Kwa mwambao wa ziwa victoria mamlaka inatarajia kutumia milioni 75 kwaajili ya kushirikiana na wananchi katika kazi tofauti tofauti zinazoendelea. Jambo linalofurahisha ni kwamba katika shule hii ya Nkilyizya hakuna mtoto anaekaa chini. Ameahidi kuendelea kushirikiana na serikali ya wilaya katika jitihada mbalimbali za maendeleo, alisema Twange.
Focus Majumbi Katibu Tawala Wilaya ametoa neno la shukrani kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa kuungana na jitihada za wilaya katika kutatua changamoto za elimu hasa katika upande wa madawati. Hali ya upungufu wa madawati ilikuwa kubwa lakini kwa sasa imeshuka na kubakiwa na madawati takribani 2000.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ukerewe Moses Nduligu amepongeza na kushukuru kwa msaada huo na kutoa rai kwa wadau wengine kuweza kujitokeza katika kusaidiana katika jitihada za kuboresha miundombinu ya elimu katika wilaya ya Ukerewe. Miongoni mwa shule za msingi zilizonufaika na mgao huo ni pamoja na Mtoni, Kakerege, Kumambe, Bukungu, Kome,, Muhula, Hamzilo, Hamkoko, Nansio, Nkilizya, Buguza, Bugorola, Halwego, Malegea, Bugula, Muriti, Nsenga, Mwigoye na Nampisi.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.