Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde Christopher E.Ngubiagai amewaasa wananchi wa Ukerewe kuendelea kudumisha amani ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuzalisha zaidi katika shughuli zao za kiuchumi ikiwa ni sehemu ya kujiletea maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na Wilaya kwa ujumla.
Akizungumza na wananchi wakati wa mkutano wa hadhara kusikiliza kero mbalimbali katika kijiji cha Muluseni kilichopo kata ya Ngoma Cde Christopher amesema ni wajibu wa kila mwanachi kudumisha amani kwenye eneo lake.
"..tunaelekea kipindi cha uchaguzi mkuu ambao utahusisha kuchagua madiwani,wabunge na Rais kila mmoja ana uhuru wa kumchagua anaemtaka ,mshindane kwa hoja na tutambue kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.."
Amewataka wananchi wa Ukerewe kuwa makini na viashiria vyovyote hatarishi vinavyoweza kudhoofisha amani iliyopo na kutoa taarifa haraka kwa vyombo ulinzi na usalama.
Aidha amewataka wazazi kuacha tabia za kutelekeza watoto na kuwalea katika misingi bora ya upendo ikiwa ni sehemu ya kupunguza matukio ya ukatili yanayoendelea ndani ya jamii.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Dkt.Dkt. Charles Mkombe amefafanua umuhimu wa watoto kupata chakula shuleni na kuwataka wazazi na walezi kuona umuhimu wa kuchangia huduma hiyo kwa ajili ya watoto wao.
Sophia Masato ni mkazi wa kijiji cha Muluseni yeye anapongeza juhudi za serikali kwa kuwajali wananchi wake kwa kuwatembelea na kusikiliza kero zao.
"Inatia moyo kwa kweli,hata kama itachukua muda angalau wametusikiliza."
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.