"..amani ndiyo mtaji wa maendeleo yetu, tukiwa wamoja hakuna jambo litakalo shindikana, Ukerewe inajengwa na sisi wenyewe kwa umoja wetu hivyo tunakila sababu ya kuilinda amani yetu.."
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cde.Christopher Ngubiagai alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bukonyo kata ya Namilembe ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara za zake za kawaida kutembelea wananchi,kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili .
Aidha amewataka wananchi hao kuwaheshimu na kuwalinda viongozi waliochaguliwa ili waweze kusimamia sheria zitakazotenda haki kwa kila mmoja hali itakayozidi kuimarisha amani na utulivu ndani ya jamii.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Ndugu Vincent Augustino Mbua amesema Halmashauri yake inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo,ili kufanikisha hilo utulivu na mshikamano ni nguzo muhimu huku akiwasihi wana Ukerewe kuwa kitu kimoja.
Senga Elisha Abeli ni Afisa ushirika wa Wilaya hiyo yeye ametoa ufafanuzi kuhusu mikopo inayotolewa na Halmashauri inayolenga kukuza mitaji na kuimarisha uchumi wa wananchi huku akiwasisitiza wananchi kufuata utaratibu uliowekwa ili waweze kunufaika na mikopo hiyo.
Veneranda Masatu mkazi wa kijiji cha Namilembe ni mkulima ameiomba serikali kuweza kutatua changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwa wakati ili kuleta usawa na kujenga mahusiano mazuri kati ya wananchi na serikali yao .
Augustino Mandago mkazi wa kijiji cha Busagami yeye amepongeza jitihada ambazo viongozi wa ngazi za juu wanazichukua kushuka katika vijiji ili kupokea na kutatua kero wanazokumbana nazo.
Cde. Ngubiagai amewasihi wananchi kuwa wa kwanza kutatua changamoto zao huku akiwataka kuheshimu maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya matumizi ya kijiji ili kuondokana na migogoro inayoweza kuepukika kwa kupanga matumizi sahihi ya ardhi yao.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.