|
|
|
Mwenyekiti wa Jumuiya ya maridhiano na amani Tanzania (JMAT) mkoa wa Mwanza Sheikh Mussa Kalwinyi amewaagiza wanaUkerewe kutetea amani ya Tanzania mahali popote watakapokuwepo bila ubaguzi wowote,wa kidini,ukabila na itikadi za kisiasa hasahasa katika kipindi hiki taifa la Tanzania linavyoelekea kwenye zoezi la uchaguzi mkuu wa Rais,wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika mnamo 29 Oktoba,2025.
".. tunawaagiza kulinda amani,tunawasha moto wa amani.."
Jumuiya ya maridhiano na amani ni taasisi iliyosajiriwa,inayofanya kazi na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikihusisha dini mbalimbali.
Akifafanua malengo ya JMAT kukutana na wajumbe wa kamati hiyo wa Wilaya ya Ukerewe Makamu mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mchungaji Josephat Magumba amesema lengo la kusanyiko hilo ni kutoa maelekezo ya kuhamasisha amani, kuhamasisha wananchi wajitokeze kwenda kupiga kura na kuliombea taifa.
"..kitu ulichonacho siku zote huwezi kuona thamani yake, amani tuliyo nayo tusiichezee kwani pindi itakapotoweka kuirejesha ni kazi,tujifunze kwa majirani zetu mataifa ambayo hayana amani tusitamani hali hiyo.." Amesema mchungaji Josephat
Nae mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe ambaye pia ni Katibu tawala wa Wilaya hiyo ndugu Allan Augustine Mhina amekemea vikali masuala ya watu kuchochea vurugu na wengine kupanga kuandamana bila kibali.
"..sisi kama viongozi wa serikali ya Ukerewe hatuko tayari kuona amani inatoweka wakati tunafahamu wapo watu ambao hawajiwezi ikitokea machafuko wengi wanaumia bila hatia.."amesema Mhina
Zainab Kimei ni mjumbe wa kamati hiyo Ukerewe, yeye amewaasa wananchi wote kuwa kitu kimoja linapokuja suala la kulinda amani.
Akihitimisha kusanyiko hilo mshauri wa JMTA mkoa wa Mwanza Sheikh Mohamed Yusuph Hassan amewaomba viongozi wa dini kuhubiri amani na kuwa washauri wazuri kwa serikali na kupinga masuala yote yanayolenga kuhatarisha amani ya taifa.
" Tanzania yetu,amani kwanza "
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.