Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye ni Katibu Tawala msaidizi Elimu ndugu Michael Ligola amewasili wilayani Ukerewe pamoja na mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu PSPF Gabriel Silayo pamoja na uongozi wa Wilaya ya Ukerewe wameshiriki katika hafla ya ufunguzi wa ofisi ya Mfuko wa pensheni kwa wafanyakazi. Hafla hiyo imefanyika katika eneo la ofisi za maliasili zamani mjini Nansio na kuhudhuriwa na wananchi na watumishi wa serikali.
Chacha Naikabwe Meneja PSPF Mkoa wa Mwanza na Mara amewasilisha mada juu ya PSPF (Public Service Pension Fund) ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria namba 2 ya mwaka 1999 iliyotokana na sheria ya mwaka 1954 ikiwa na majukumu kama kutambua na kusajili wanachama, kuwekeza michango inayokusanywa,kukusanya michango kutoka kwa mwajiri 15% na 5% mtumishi, kulipa mafao, kutunza kumbukumbu za wananchama na kutoa elimu ya mafao.
Gabriel Silayo mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu PSPF ameeleza kuwa imekua ni jambo jema Ukerewe kupata ofisi kwani ni eneo leny changamoto ya kijiografia na kuna wanachama wanaochangia hivyo ameahidi kuwa ofisi hiyo itatoa huduma njema bila kupata adha ya kwenda Mwanza. Silayo ameeleza kuwa wilaya ya Ukerewe imepata upendeleo kuwa kati ya miongoni mwa Wilaya chache zilizobahatika kupata Ofisi ikiwemo Pemba, Zanzibar na sehemu nyingine, kwani kwa sasa ofisi zipo katika ofisi za mkoa wa Mwanza.
Michael Ligola Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza akitoa hotuba amepongeza sana Mfuko wa PSPF kuwa mfuko wa kwanza kufungua na kusogeza huduma za ofisi katika wilaya ya Ukerewe ili kuweza kupata huduma kwa karibu kama wanavyoweza kupata watanzania wengine. Kwa maana hiyo inatekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya PSPF pamoja nawe. “Nina imani kuwa huduma zote za mfuko zitapatikana Ukerewe” Ligola. Ametoa rai kuwa mfuko utoe elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya mifumo miwili ya uchangiaji yaani ule wa uchangiaji wa hiari kwa wananchi wote na ule wa sekta za ajira rasmi. Hivyo amewataka wananchi wa Ukerewe kuchangamkia fursa ili kunufaika na mafao na huduma za PSPF.
Ligola amewataka waajiri kuchangia watumishi wao kwa wakati ili kuwaepushia wale watakao kuwa wakistaafu kushindwa kulipwa mafao yao, hivyo amesisitiza kuwa ni swala baya kwani ni kuwatesa wastaafu pasipo sababu. Kauli mbiu ya Mfuko wa pensheni wa PSPF katika kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja mwaka huu ni Tunasikiliza Tunakujali, PSPF pamoja nawe.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.