Katibu Tawala wa Wilaya ya Ukerewe ndugu Focus Majumbi amekabidhi kadi za CHF iliyoboreshwa kwa kaya za watu wenye ualbino ambapo kaya 25 zimekabidhiwa vitambulisho hivyo katika ukumbi wa Albino uliopo bukongo ambapo kila kaya inakuwa na wategemezi 6 watakao tibiwa kupitia CHF.
Majumbi amepongeza kwa hatua hiyo kwani vitambulisho hivyo vitawawezesha watu wenye ualbino zaidi ya 36 kutoka katika kaya 25 kupata matibabu katika hospitali mbalimbali tofauti na hapo awali walikua wakitibiwa katika zahanati pekee.
Ramadhani Halfan Mwenyekiti wa Chama cha watu wenye Ualbino Ukerewe ameshukuru kwa ushirikiano unaoendelea kutolewa na wadau mbalimbali hapa wilayani na nje. Kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali kama LILIAN Foundation na KCBRP limewawezesha kutoa elimu katika kukusanya makundi mbalimbali katika jamii na kutoa elimu ya kuondoa unyanyapaaji.
Aidha Focus Majumbi amekabidhi vifaa vya kujikinga jua kwa kaya za watu wenye ualbino ili kuwakinga na mionzi ya jua, vifaa hivyo vimetolowa na LILIAN Foundation kupitia Karagwe Community Based Rehabilitation Program mradi ulioanza mwaka 2017 na unatarajiwa kuisha January 2020 umewezesha kupatikana kwa vifaa hivyo ambavyo ni kofia 90, miamvuli 90, mabegi 90 vyenye thamani ya Tsh. 2,070,000/-.
Ignant Kapira Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ukerewe ameahidi kuendelea kuhakikisha watu wenye ualbino hawapati adha yoyote, kwa kuangalia usalama na kupambana na wote wanaowatishia kwa namna moja au nyingne . ameeleza polisi ina dawati maalum kushughulikia matukio ya namna hiyo hivyo amewaondolea hofu. Amepongeza wanaukerewe na kuwataka kuendelea kuwalinda watu wenye ulemavu kwani ni miaka miwili tangu aripoti Ukerewe hakuna tukio baya lililoripotiwa.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.