Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mhe. Joshua Bituro Manumbu Diwani wa Kata ya Igalla (CCM), amefanya ziara ya kikazi katika kisiwa cha Ukara kwa siku tatu (3), lengo likiwa ni kukagua miradi ya Maendeleo inayotekelezwa katika tarafa ya Ukara. Miradi yote inayotekelezwa tarafa ya Ukara inajumla ya Tsh. 246,301,900.00. Miradi inayotekelezwa tarafa ya Ukara ni katika sekta ya elimu na afya ambapo fedha zinazotumika kutekeleza miradi hiyo zinatoka mapato ya ndani, Ruzuku ya Serikali kuu, P4R, na CDCF.
Mhe. Manumbu akiwa ameambatana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji (W) Bw. Goodluck Mtigandi kutembelea miradi mbalimbali ya Maendeleo ikiwa ni pamoja na Mradi wa Ukamilishaji vyumba viwili vya madarasa Shule ya Msingi Kumambe ambapo wamekmilisha madarasa mawili na ofisi moja na vyoo vyenye matundu 11 kwa thamani ya shilingi Milioni 48.8 na choo kiko katika hatua ya ukamilishaji fedha kutoka P4R.
Mradi wa Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa shule ya Sekondari Bwisya wenye thamani shilingi Milioni 40 fedha kutoka P4R Mradi ambao mpaka sasa uneshakamilika na madarasa hayo yanatumika na wanafunzi wa shule hiyo. Mradi wa Ukamilishaji wa vyumba viwili vya maabara ya Sekondari ya Bukiko kwa Shilingi Milioni 60 ikiwa na Ruzuku kutoka Serikali Kuu, katika mradi sekta ya afya CDCF imetoa kiasi cha Milioni 10 kutekeleza ujenzi wa jingo la Zahanati ya Kome Mradi.
Mhe. Manumbu amewapongeza wote kwa kusimamia na kutekeleza miradi hiyo ambapo thamani ya Fedha inaonekana. “Ubora wa miundombinu ndio utaofanya miradi hii kudumu muda mrefu, tunzeni miundombinu hii ili iwafae wengi” alisema Manumbu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bw. Goodluck Mtigandi amewataka wasimamizi wa miradi hiyo kufanya kazi kwa ukaribu ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati ili ianze kuhudumia wanaohusika.
Aidha katika hatua nyingine Mhe Manumbu amezungumza na wananchi wa Bwisya katika mkutano wa Hadhara lengo likiwa kusikiliza kero za wananchi. Ambapo akijibu changamoto za wananchi waliouliza juu ya michango yao ya ujenzi wa Shule ya Msingi Bwisya ambapo baada ya kukagua shule hiyo aliagiza mapato na matumizi ya makusanyo hayo kusomwa katika kikao hiko na kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji (W) kuleta Mkaguzi wa Ndani kufika na kukagua Fedha zote za Mradi huo na kuwasilisha taarifa hiyo. Shule ya Msingi Bwisya ilichangisha michango ya wananchi takribani milioni 10 na kupatiwa Ruzuku ya Serikali Kuu milioni 12.5.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Joshua Bituro Manumbu ameendelea na ziara katika kisiwa cha Ukara ambapo ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata za Nyamanga na Bukungu.
Kata ya Nyamanga amekagua Shule ya Sekondari ya Nyamanga iliyofunguliwa 17/2/2019 na sasa wananchi wanajenga madarasa mawili na ofisi moja. Amewapongeza wananchi kwa juhudi hizo amewataka waendelee kushiriki shughuli za Maendeleo na serikali itakamilisha.
Kata ya Bukungu katika Shule mpya ya Sekondari walipatiwa milioni 25 za mapato ya ndani ya Halmashauri ili kujenga vyumba vinne vya madarasa na Mpaka sasa ujenzi huo unaendelea. Amewasihi wanabukungu kuongeza nguvu ili shule hiyo ianze kazi na kupokea wanafunzi.
Aidha katika Shule ya Msingi Bukungu wamejenga vyoo matundu 20 ambapo matundu ya kiume ni 10 vya kike ni 10 matundu hayo yanajengwa kwa Nguvu za wananchi Kijiji cha Bukungu. Matundu hayo yatawahudumia wanafunzi 1379 katika Shule hiyo.
Manumbu amewapongeza sana kwa ujenzi huo na ameelekeza tundu moja litengwe kwa wenye mahitaji maalumu. “Nawapongeza sana wana Bukungu kwa ujenzi wa choo, tutatafuta Fedha tuwaunge mkono” Alisema Manumbu.
Mwenyekiti wa kijiji Bukungu Mhe. Etami Machungwa ameeleza lengo ni kuondoa adha ya upungufu wa matundu ya choo shuleni hapo na kama kijiji kwa kushurikiana na uongozi wa shule tumeweka nia ya kukamilisha mradi huu wa choo kufikia mwezi June mwaka huu.
Goodluck Mtigandi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri amewapongeza sana wananchi hao kwa hatua hiyo na Amehamasisha wananchi kuendelea kujitoa na kuibua miradi na kuitekeleza kwa ubora.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.