Katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya Ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya Bi. Zubeda Kimaro akiwa na kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, wakuu wa Idara na vitengo, wakuu wa taasisi mbalimbali, viongozi wa chama, kata, kijiji na wananchi wamejitokeza na wameshiriki zoezi la upandaji Miti 680 katika shule mpya ya wasichana Ukerewe iliyopo kata ya kagunguli Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza kwa lengo la kuhifadhi mazingira na kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kushiriki zoezi hili katika eneo la Shule ya wasichana Ukerewe iliyopo kata ya Kagunguli wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Bi. zubeda Kimaro amewaagiza viongozi walezi wa kata zote kusimamia zoezi la upandaji miti katika taasisi za serikali zilizo katika maeneo yao ili kufikia lengo la kupanda Miche elfu tano kwa Wilaya nzima ya Ukerewe.
Aidha, Bi. Zubeda amewaomba wananchi kushiriki zoezi la kupokea chanjo ya uviko 19 linalo endelea kutolewa wilayani hapo na kufafanua kuwa chanjo hiyo ni salama na haina madhara yoyote kwa mwananchi.
Kwa upande wake Afisa Misitu Wilaya ya Ukerewe Goodluck Mtigandi ameeleza kuwa, kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita halmashauri ya wilaya ya Ukerewe imefanikiwa kupanda miti laki mbili, hamsini na saba elfu na mia tano katika hekta elfu mbili kumi na saba tu, miti hiyo imepandwa katika hifadhi za serikali, Misitu ya jamii, taasisi za umma pamoja na maeneo ya watu binafsi miti ambayo imetolewa na TFS.
Kwa mwaka 2021 halmashauri ya wilaya ya Ukerewe imepanda jumla ya miti laki moja arobaini na moja elfu katika maeneo mbalimbali Wilayani hapo.
Afisa Misitu Mtigandi ameelezea mpango wa halmashauri kwa mwaka 2021 kuwa inatarajia kupanda hekta mia tisa tisini na saba katika maeneo ya wilaya nzima hasa maeneo yasiyo na miti katika kisiwa kikubwa cha Nansio, Kisiwa cha Ukara, kisiwa cha Irugwa na kisiwa cha Bwiro ikiwa ndiyo maeneo yaliyopewa kipaumbele.
Aidha Bi. Zubeda ameshukuru Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Hapa Wilayani Ukerewe na Shamba la miti Rubya kwa juhudi wanazozionesha kuhakikisha miti mingi inaendelea kupandwa katika Wilaya ya Ukerewe na utoaji wa Elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa Miti na utunzaji mazingira.
KAULIMBIU "Miaka 60 ya Uhuru, Tanzania imara na kazi iendelee".
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.