Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Ndugu Josephat Mazula amewataka wananchi wa Ukerewe kuwa mstari wa mbele kutumia fursa ya uwepo wa chuo cha ufundi stadi VETA kilichopo kata ya Bukanda kijiji cha Muhula kwa kupeleka wanafunzi wengi wazawa kwani ujuzi haupotei na uumpa uwanda mpana mwenye nao kuamua nini cha kufanya kujiimarisha kiuchumi.
Ameyazungumza hayo wakati wa hafla ya kutuku vyeti kwa wanafunzi 22 wa kozi za muda mfupi waliohitimu mafunzo ya fani mbalimbali za ushonaji, umeme,mabomba na kompyuta.
"..Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza na kuboresha miundo mbinu wezeshi kwa ajili ya kupata mafunzo ya ufundi katika nyanja mbalimbali.Hapa Ukerewe tayari tunacho chuo kizuri kabisa cha VETA mnakokwenda mkawe mabalozi wazuri kwa kutumia ujuzi wenu ipasavyo.."
Nae Mkuu wa chuo hicho Mhandisi Deusdedith Shinzeh amesema viongozi na watumishi wa chuo hicho wamepewa dhamana kubwa na kuweka wazi uwepo wa wanafunzi wenye digrii ambao wanatekeleza agizo la waziri Mkuu kuhusu kuongeza ujuzi katika taaluma zao.
Amri Bushiri ni mkufunzi wa somo la stadi za maisha na masuala ya afya ya uzazi na UKIMWI na ujasiriamali somo ambalo ni lazima kwa fani zote anasema mbali ya kuwaandaa wanafunzi na ufundi chuo kiliona umuhimu wa wanafunzi wote kupata elimu ya kujitambua miili yao sambamba na kuwawezesha kupambana na mazingira tofauti tofauti katika kuishi kwao.
Michelle Moris ni miongoni mwa wahitimu kutoka mkoa wa Mara katika fani ya ushonaji anapongeza uongozi wa chuo kwa mafunzo na miongozo mizuri walioipata chuoni huku akiahidi kuwa balozi mzuri.
Akihitimisha hafla hiyo ndugu Mazula amesisitiza jamii kuona umuhimu wa elimu kwani ni msingi wa kila kitu na kuwataka wahitimu hao kuwa chachu ya mabadiliko katika maeneo waliyotoka ili kuwa na kesho bora.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.