"..ulinzi wa taifa letu ni jukumu la kila mtanzania, kila kijana anatakiwa kushiriki katika ulinzi endapo nchi itakuwa matatani uwepo wa jeshi la akiba ni kwa ajili ya kuimarisha amani na utulivu ndani ya jamii.."
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde, Christopher Ngubiagai alipokuwa akifunga mafunzo ya jeshi la akiba yaliyojumuisha kata za Namilembe, Kakukuru na Ilangara ambapo askari 72 wamehitimu mafunzo hayo yaliyohitimishwa leo katika kijiji cha Nakamwa kata ya Namilembe wilayani Ukerewe.
Akisoma taarifa ya mafunzo hayo Kaimu mshauri wa jeshi la akiba Wilaya ya Ukerewe Nyamsha Mnene Dioniz amesema mafunzo yalianza rasmi tarehe 22/04/2025 yakiwa na idadi ya wanafunzi 58 na kufungwa rasmi leo tarehe 24/09/2025 yakiwa na jumla ya wanafunzi 72.
Ameongeza kuwa wanafunzi hao wamejifunza masomo mbalimbali ikiwemo utimamu wa mwili, usomaji wa ramani, uhamiaji,kuzuia na kupambana na rushwa, ujanja porini, zimamoto, sheria za jeshi la akiba na mbinu za kivita ili wawe tayari kwa dharura zozote za kitaifa lakini pia kuongeza wananchi ambao wapo tayari kulinda amani ya taifa.
Mhe.Ngubiagai amewataka wahitimu hao kuwa mabalozi wa nidham, maadili kwa lengo la kujenga taifa lenye mshikamano.
Paredi kamanda wa jeshi la akiba John Matondane Denis ni miongoni mwa wahitimu amewasihi vijana wenzake waliopo mitaani kujiunga na jeshi la akiba na waondoe fikra potofu kwamba kuingia mgambo ni kushindwa maisha kwani tayari yeye ana ujuzi ambao anaweza kutumia sehemu mbalimbali akihitajika .
Mbali na kufunga mafunzo hayo Cde, Ngubiagai amewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni za wagombea na kupiga kura katika uchaguzi mkuu inayotarajiwa kufanyika Oktoba 29 2025.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.