Wananchi wanaoishi maeneo ya visiwani wilayani Ukerewe wanatarajia kunufaika na huduma ya nishati ya umeme. Nishati hiyo ya umeme jua inayowezeshwa na mwekezaji Rex Energy ambao unatakuwa ni moja ya kichocheo cha uchumi wa maeneo mengi ya visiwa katika wilaya ya Ukerewe na hii ni baada ya kufanya uzinduzi wa mradi huo wa umeme katika kisiwa cha Gana, uliohusisha wananchi waliojitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo lililoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Frank S. Bahati na Mkurugenzi mkuu wa Rex Energy Francis Kibhisa ambaye ndio mwekezaji.
Utekelezaji wa mradi wa nishati ya umeme jua unatakuwa wa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza imeanza agosti 2016 na kukamilika desemba 2017, ambapo miundombinu imefikia hatua nzuri na visiwa vitakavyo nufaika na awamu hiyo ni Gana, Bwiro, Kamasi, na Bulubi. Katika awamu ya pili mradi utakamilika mwaka 2018 ambapo na kunufaisha visiwa vya Kweru kubwa, Kweru mto,Siza, Bushingere, Izinga na Sizu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Frank S. Bahati ameshukuru Rex Energy kwa kuwekeza nishati ya umeme jua katika visiwa kumi vya Ukerewe. Kupatikana kwa umeme katika maeneo ya visiwa utasaidia kukuza uchumi hasa wa viwanda kwani ni adhma ya serikali ya awamu ya tano kuwa na uchumi wa viwanda. Umeme utawasaidia vijana kujishughulisha na kazi mbalimbali, pia mradi utakua msaada kwa shule,vituo vya afya na taasisi za kidini. Amewataka wananchi kuupokea kwa mikono miwili mradi na kushirikiana kuutunza kuhakikisha unakuwa msaada kwa vizazi na vizazi.
Mkurugenzi mkuu wa Rex Energy Francis Kibhisa ameshukuru Serikali kuanzia Wizara ya Nishati na Madini, Rea na serikali ya Wilaya ya Ukerewe kwa kutoa ushirikiano wa kufanikisha mradi huo kuanza kufanya kazi katika visiwa vya Ukerewe, baada ya miezi miwili umeme utakuwa umewashwa. Baada ya mradi kuanza kazi kuna maeneo ambayo itashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kuboresha maeneo makuu matatu ambayo ni Elimu na kuimarisha majengo ya shule na vyoo kama ambavyo wamesaidia ujenzi wa choo cha shule ya msingi Miti mirefu, Afya kuanzisha kituo cha afya au zahanati, usalama kuweka kituo cha polisi.
“Gharama za mradi ni bilioni 18 hadi 21 ambazo ni sawa dola milioni 9 hadi 11 za kimarekani” alisema Kibhisa. Mradi utakuwa wa manufaa zaidi kwa vijana wengi watapata mafunzo na kuajiriwa katika kazi mbalimbali za Rex Energy. Ametoa rai kwa watanzania kuwekeza ndani ya nchi kama alivyofanya yeye na kuwa maendeleo ya nchi yanaletwa na watanzania wenyewe na kutokata tama katika kusaidia serikali.
Umeme jua wa Rex Energy unatarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi ya 5000 na itavutia wafanyabiashara wengi kutumia fursa na kujiongezea pato na wametakiwa kushirikiana na mwekezaji kutunza miundombinu.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.