Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mhe.Cornel Magembe ahamasisha kilimo cha machungwa kwa wakulima wa Wilaya hiyo kwani ni moja ya kilimo biashara chenye tija kuanzia kwa mkulima hadi taifa, ameyasema hayo akifungua mkutano wa wadau wa machungwa, katika Ukumbi wa Albino ulioandaliwa na MVIWAU chini ya ufadhili wa VI Agroforesty na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. George Nyamaha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ester Chaula, waheshimiwa madiwani, wakuu wa Idara na taasisi za kifedha.
Magembe ametoa rai kwa wakulima na wadau hao kufuata kanuni na taratibu muhimu za kilimo hiko cha machungwa ili kuweza kupata mazao bora na ya kutosha. Amesikitishwa na uuzaji wa machungwa ambayo bado matunda hayajakomaa na kufanya hivyo inaumiza mkulima. Baadhi ya kanuni na taratibu hizo ni utunzaji wa mimea hiyo uchaguzi wa mbegu bora na ushirikishwaji wa wataalamu wa kilimo juu ya uangalizi wa mimea hiyo.
Magembe amewataka maafisa ugani kutokaa maofisini tu bali kutoka na kusambaa sehemu mbalimbali katika kata zao ili kutoa ushauri wakitaalamu juu ya kilimo na kuwezesha kilimo bora kitakachoweza kukidhi haja ya mkulima kiuchumi na kuongeza chachu ya maendeleo ya wilaya. “Serikali itahakikisha kuzidisha mchango wake katika sekta ya kilimo”.Alisema Magembe katika mkutano huo na kuzidi kuhamasisha kwamba si mimea ya michungwa pekee bali hata mimea ya matunda mengine ili kukidhi haja ya viwanda vya Tanzania na wawekezaji kwa ujumla.
Magembe pia amekemea tabia ya wakulima hao ya kuuza miche michanga ya mimea ya michungwa bila kuangalia faida ya mbeleni ya uzao wa mimea hiyo na matokeo yake kuiuza kwa bei ya chini sana na kupelekea kudumaa kiuchumi .Hivyo amehakikisha kukomesha tabia hiyo ya wakulima na kushauri zao hilo kuwa zao la biashara wilayani humo.
Kent Larsson Meneja Mkazi wa Shirika la VI Agroforesty lenye makao yake makuu nchini Sweden ambao ni wafadhili wa Shirika la Muungano wa Vikundi vya Wakulima, Wavuvi na Wafugaji Ukerewe (MVIWAU), amesema Shirika hilo limeonesha mchango wake katika kilimo ikiwa na utoaji bure wa elimu ya kilimo,ushauri wa mbegu bora za mimea ya bustani hususani michungwa ikiwa lengo lao kubwa mbali na kupiga vita umaskini wa wakulima bali pia ni kuiunga mkono serikali katika kilimo cha mimea ya matunda wilayani humo kupitia miradi mbalimbali kama ALIVE [Agoforesty For Livelihood Empowerment]ulioanzisha wilayani humo.
Larsson ameeleza kuwa uboreshwaji wa fursa mbalimbali kwa wakulima ili kuboresha kilimo cha zao la machungwa na matunda kwa ujumla ili kuwakwamua wakulima kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi hasa wakulima wa Ukerewe.
Aidha mashirika ya kifedha na vikundi mbalimbali kama NMB Bank [National Microfinance Bank] na Ukerewe SACCOS yameonyesha mchango mkubwa kwa wakulima kwa kuwawezesha mikopo ili kuendeleza kilimo bora na chenye tija.
Wakulima katika mkutano huo wameiomba Halmashauri ya wilaya hiyo kuimarisha mipango mikakati ya biashara na kilimo kwa ujumla ili kuimarisha kilimo cha machungwa kilicho bora na kukidhi uchumi wa wakulima na jamii za Wakerewe kwa ujumla.
Paulin Makubi Mwenyekiti wa MVIWAU ameshukuru shirika la VI Agroforesty kwa kuendelea kushika mkono kilimo katika Wilaya ya Ukerewe, pia ameshukuru Halmashauri kwa kuendelea kutoa ushirikiano. Ameomba wakerewe kuanza kujihususha na ufugaji wa samaki ndani ya ziwa kwani ni chanzo kizuri cha uchumi.
Gregory K. Gabriel, Diwani wa kata ya Bukindo na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe amewataka wakulima wa machungwa kufanyia kazi maelekezo na ushauri wa wataalamu wa kilimo na kuongeza tija na thamani katika kilimo cha matunda, amewapongeza na kuwashukuru shirika la VI Agroforesty kwa kuendelea kujali uchumi wa ukerewe kwa kutoa mafunzo na fursa za kilimo hasa machugwa na upandaji miti kwa zaidi ya miaka 20 sasa kwani imesaidia utunzaji wa mazingira kwa kiasi kikubwa.Amesema hayo wakati wa kufunga mkutano huo wa wadau wa kilimo cha machungwa.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.