Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde Christopher E.Ngubiagai amewaalika wadau mbalimbali nje na ndani ya Ukerewe kuja kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita katika mapambano dhidi ukatili kwa watoto.
Ameyazungumza hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yanayoadhimishwa kila mwaka Juni 16 ikiwa ni ishara ya kuwakumbuka zaidi ya watoto 100 waliouwawa katika maandamano ya amani Soweto nchini Afrika ya kusini walipokuwa wakidai haki zao za msingi ikiwemo elimu bora.
" Migogoro ya kifamilia imekuwa ikiwaathiri watoto kwa kiasi kikubwa sana kiasi cha kusababisha watoto kujiingiza katika makundi na tabia zisizofaa, wazazi mpunguze ubize wa kutafuta maokoto zungumzeni na watoto wenu.." Amesema Cde Ngubiagai
Akichangia katika mdahalo wa malezi ya watoto Shekhe wa Wilaya ya Ukerewe Shabani Hugo John amesema ni muhimu watoto wafundishwe hofu ya Mungu toka wanapokuwa wadogo kwani itawapa mipaka pale wanapotaka kufanya jambo lolote katika kuishi kwao.
Bernadetha M.Daud ni Mkuu wa dawati la jinsia na watoto katika Wilaya ya Ukerewe amewataka watoto kujilinda kwa kukataa kufanyiwa vitendo hatarishi na wasinyamaze wanapofanyiwa ukatili wa aina yoyote .
Nae Ester Nyanda mwanafunzi wa darasa la 7 akiwa ni mmoja wa washiriki katika bunge la watoto amezitaja haki za mtoto ikiwa ni pamoja na haki ya kuendelezwa kielimu,kulindwa,kutobaguliwa na kushirikishwa katika maamuzi.
Akihitimisha hafla ya maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe.Manumbu ameishukuru idara ya maendeleo ya jamii kwa kuratibu vyema sambamba na kupongeza hatua kubwa ya mafanikio ambayo imefikiwa na Halmashauri hiyo.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.