Kina mama wajawazito Wilayani Ukerewe wameshauriwa kuwahi Kliniki punde wanapojigundua na kuona dalili za ujauzito ili kupata vipimo, ushauri na dawa kinga muhimu kwa ajili ya ukuaji mzuri wenye afya kwa wote mama na mtoto.
Akitoa elimu wakati wa Kliniki ya Baba, Mama na Mtoto Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe (Bomani) Jesca Majura amewahimiza akina mama waliofika kliniki kwa ajili ya huduma mbalimbali kuanza mapema kliniki kwa kuzingatia umuhimu na faida nyingi zinazopatina .
".. inasaidia kufahamu afya ya mama na mtoto, kupata huduma za mapema kama chanjo, vipimo, ushauri, dawa kinga na matibabu ya haraka pale inapolazimu kufanya hivyo hali inayomuwekea mama mazingira rafiki ya kujifungua salama mtoto mwenye afya.
Aidha amewaasa wajawazito kupata matibabu ya magonjwa ya zinaa kama Kaswende, Maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi na Malaria kwani ni magonjwa yanayoweza kumuathiri mtoto akiwa tumboni au wakati wa kuzaliwa huku akiwasihi kina mama hao kuachana na imani potofu pale mtoto anapozaliwa na changamoto ya kichwa kikubwa au mgongo wazi kwa kutambua hayo ni miongoni mwa madhara ya mama mjamzito kuchelewa kuanza kliniki .
Salome Mathiasi Mchele ni mkazi wa kijiji cha Bukongo kata ya Bukongo yeye amepongeza utolewaji wa elimu hiyo kwa wazazi kwani imewawezesha kufahamu kuwa hata vyanzo vingi vya vifo vya watoto wachanga vinatokana na mama mjamzito kuchelewa kuanza huduma za kliniki hiyo.
"..Muende mkawe mabalozi wazuri huko majumbani na muwasisitize wamama waje mapema ,zipo dawa kinga ambazo mama anaweza kutumia pale anapotaka kupata ujauzito ambazo zitamkinga na maradhi na atakuwa salama mpaka kujifungua.."
Doris Elias mkazi wa kijiji cha Kagera anasema amenufaika na elimu hiyo na kwamba hatokosa kliniki hata siku moja ataenda na ratiba zitolewazo na wauguzi kwani anatamani kupata mtoto mwenye afya nzuri.amewaomba wazazi wote kuzingatia Kliniki na kufuata utaratibu wote kwa mujibu wa ratiba zitolewazo na wauguzi hospitalini hapo.
Akihitimisha elimu hiyo Jesca Majura amesema hakuna sababu yakuruhusu mama mjamzito apate changamoto zinazoweza kuzuilika kwa kuwahi kliniki.
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.