Tume ya utumishi wa walimu (TSC) Ukerewe imetoa mafunzo elekezi kwa jumla walimu 131 ajira mpya waliohudhuria mafunzo hayo ambapo walimu 75 ni wa shule za sekondari na 56 shule za msingi ndani ya Wilaya ya Ukerewe.
Akifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa shule ya sekondari Bukongo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Ndugu Vicent Mbua amewataka walimu kufanya kazi kwa bidii na kutambua thamani ya wao kuwepo kwenye nafasi hizo.
"..wote mnafahamu bado serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri katika kuhakikisha kila mwanachi anapata cha kufanya, sio wote mliomaliza nao wamepata kazi.Ni wakati wenu kuthamini mlichonacho kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi mkidimu katika kanuni na miongozo mbalimbali ya kiserikali.Ualimu ni wito muwe tayari kutumikia umma kwa uadilifu.."
Nae Stephen Kushoka Katibu msaidizi TSC Wilaya ya Ukerewe amewafahamisha walimu hao muundo,historia na majukumu ya tume ya utumishi wa walimu (TSC) huku akiwasisitiza kubadili mtindo maisha kwa kuachana na mambo yasiyofaa na kuvaa uhusika wa mtumishi wa umma kwa kuwa na haiba nzuri wakati wote .
Akitoa mada ya haki na wajibu kwa walimu hao Afisa ajira TSC Ukerewe Bi.Magreth Nyanyusa amewataka walimu kuzingatia sheria,kanuni,taratibu na miongozo inayosimamia utumishi wao wakati wote wa ajira.
Tutayo Siloma ni mwalimu ajira mpya katika shule ya sekondari Pius Msekwa iliyopo kata ya Mulutunguru yeye anaahidi kuwa bora katika kazi yake.
".. Hapa ni kufanya kazi nzuri tu ndicho kitu pekee kitakachotuuza vinginevyo maneno hayasaidii.."
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.