Walimu wakuu wateule wametakiwa kuimarisha umoja na mshikamano kwa watu wanaokwenda kuwaongoza, lengo la kikao hicho ilikuwa kuwakumbusha walimu hao kuhusu maadili, mahitaji ya mtaala mpya na miongozo juu ya utendaji kazi katika vituo walivyopangiwa.
"... nendeni mkaimarishe umoja na mshikamano kwa kundi mnalokwenda kulisimamia, mkaboreshe kwenye mapungufu mkawe makini katika kufanya maamuzi yatakayoleta manufaa kwa jamii inayowazunguka..." Amesema Rasuli Amir Mbwambo- Kaimu Afisa elimu msingi.
Kwa upande wake Afisa uthibiti ubora wilaya ya Ukerewe Mwl. Misana Nyasani Maige amewataka walimu hao kuzingatia maelekezo ya mtaala mpya wa elimu ikiwa ni kuwa na Mihitasari, miongozo ya ufundishaji, vitabu vyenye ithibati, maazimio ya kazi, maandalio ya masomo, shajala ya masomo, shajala ya vipindi na kuunda vyama vya masomo kupitia idara ya ndani ya uthibiti ubora vitakavyowaongezea weledi katika utendaji .
Nae Katibu msaidizi tume ya utumishi wa walimu Mwl. Richard Edward Shaban amewasihi walimu hao kujibidisha kufahamu kanuni, miongozo na sheria ambazo zitawasaidia kuwaongoza katika kusimamia maadili na nidhamu kwa kundi wanalokwenda kulisimamia huku akiwataka kujiweka kando na masuala ya utovu wa nidhamu ili kulinda heshima zao kama viongozi.
Mwalimu Luchagula Masanja ni mwalimu mkuu wa Shule ya msingi Bukiko amewasihi walimu wenzake kushirikisha walimu wao katika mambo mbalimbali kwa ajili ya kutanua uelewa na kuondoa tofauti zinazoweza kujitokeza huku akiwaomba kuendana na mazingira ili kurahisisha utendaji kazi.
Akihitimisha kikao hicho Mbwambo amewataka walimu hao kuiunganisha jamii na taasisi, kutengeza motisha zitazowavutia walimu wengine kujiunga na shule zao huku akiwaasa kuongeza umakini katika kusimamia miradi na vifaa vinavyotolewa na serikali katika shule wanazoziongoza ili kuleta maendeleo katika taasisi hizo.
Jumla ya walimu wakuu 15 wameteuliwa.
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.