Katika kuadhimisha siku ya lishe kitaifa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kupitia kitengo cha lishe imeendelea kutoa elimu ya lishe kwa wananchi kupitia jiko darasa, shughuli iliyowaleta pamoja kina mama, wazazi na wadau wa afya ambao wamepatiwa maarifa kuhakikisha familia zinapata mlo kamili unaochangia ukuaji na ustawi wa jamii.
Akizungumza katika kijiji cha Kitanga kata ya Kakukuru Afisa lishe wilaya ya Ukerewe ndugu Ditram Kutemile amesema lengo la jiko darasa ni kuwajuza wananchi jinsi ya kuandaa chakula chenye virutibishi kwa viwango vinavyotakiwa.
"... lengo la jiko darasa ni kuboresha mapishi na ulaji bora wa virutubishi kwa kuzingatia makundi yote ya vyakula ili kujenga uimara wa afya kwa jamii..." Kutemile.
Akitoa mafunzo juu ya makundi ya vyakula Afisa lishe hospitali ya wilaya Nansio Bi.Julieth Peter amewaasa wananchi kuzingatia makundi ya chakula ambayo ni vyakula asili ya wanyama, jamii ya mikunde, mbogamboga, matunda na mafuta yasiyo na madhara ili kutengeneza lishe bora.
Annastazia Lusato ni mkazi wa kijiji cha Kitanga yeye anapongeza serikali kwa jitihada kubwa wanazozifanya kuhakikisha wanatengeneza jamii yenye afya njema kupitia elimu ya jiko darasa kwa wananchi.
Revocatus Matage mkazi wa kijiji cha Mibungo amewashukuru wataalam hao wa afya huku akiwasihi wananchi kufuata maelekezo ya mafunzo hayo ili kutengeneza kizazi imara .
Akihitimisha zoezi hilo ndugu Kutemile amewaasa wananchi hao kuwa mabalozi wazuri kwa kuhamishia elimu hiyo katika familia zao ili kupunguza adha ya magonjwa mbalimbali yanayoweza kuepukika kwa kuzingatia lishe bora.
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.