Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde.Christopher Ngubiagai amewaasa wananchi wa Ukerewe kuendelea kushiriki shughuli za maendeleo kwani maendeleo ndani ya jamii yanaletwa na jamii yenyewe.
Ameyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi hati ya kukamilisha mradi wa TASAF wa ujenzi wa bweni la wasichana lenye uwezo wa kutoa huduma ya malazi kwa wanafunzi 80 katika shule ya sekondari Mibungo kwa jamii ya kijiji cha Mibungo kata ya Kakukuru.
“..hatuna budi kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa mapambano anayoendelea nayo dhidi ya umaskini kwa kutoa fedha nyingi za miradi kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF..”
Akisoma taarifa ya mradi huo mratibu wa TASAF Ukerewe Bi .Jenitha Byagalama amesema Halmashauri ilipokea jumla ya kiasi cha shilingi 162,954,748.37 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana ,utengenezaji wa vitanda 80 na uvunaji wa maji lita 10,000.
Miradi mingine iliyokabidhiwa hati za kukamilisha mradi ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa afya (2 in 1) iliyotengewa fedha kiasi cha shilingi 92,084,009.74 katika kijiji cha Bwasa kata ya Igalla pamoja na ujenzi wa bweni la wavulana iliyotengewa jumla ya kiasi cha shilingi 162,111,099.84 katika shule ya sekondari Illangala iliyopo kijiji cha Gallu .
Ahazi Malegesi ni mwanafunzi katika shule ya sekondari Mibungo yeye anashukuru kwa uwepo wa bweni la TASAF shuleni huku akikiri kuwa litaleta manufaa makubwa kwa watoto wa kike na kuwapunguzia vishawishi vya njiani na mimba zisizotarajiwa.
Aidha Mhe.Ngubiagai ametembelea miradi mingine miwili inayoendelea ya ujenzi wa zahanati ya kijiji Kakerege ndani ya kata ya Kakerege na zahanati ya kijiji cha Chabilungo ndani ya kata ya Mkituntu na kupongeza nguvu ya wananchi yenye mchango mkubwa katika kufanikisha miradi huku akiwataka wananchi kuthamini mchango wa serikali wa uwekezaji mkubwa kupitia TASAF kwa kulinda miundo mbinu yote na kuhakikisha inatumika kwa usahihi.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.