Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cde, Christopher Ngubiagai amewataka wananchi kuimarisha amani na mshikamano wa kijamii ili kuchochea maendeleo hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu .
Ameyasema hayo katika kijiji cha Mulutilima kata ya Kakukuru alipokuwa akizungumza na makundi mbalimbali ya vijana, wanawake, wavuvi, wazee maarufu, viongozi wa dini,wenyeviti wa vijiji na vitongoji, viongozi wa vyama vya siasa ,wanamichezo,waganga wa tiba asilia, wamiliki wa vyombo vya usafiri,wajasiriamali na wafanyabiashara.
".. tuna ziwa kwa nini tuwe maskini,ni muda sasa wa kutumia rasilimali tuliyonayo kuchochea maendeleo." Cde, Ngubiagai
Aidha, amewasihi wajasiriamali na wafanyabiashara kufahamu thamani ya nidhamu ya fedha kama kutunza mtaji, kuendesha biashara kwa mahesabu sahihi, kuongeza ujuzi pamoja na kuweka akiba na kuwekeza ili kutokuyumba kibiashara na kurejesha kwa wakati mikopo ya asilimia 10% inayotolewa na Halmashauri.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Vincent Mbua amewataka wananchi kuendelea kuinua uchumi kwa kulipa kodi na tozo mbalimbali ili kukuza mapato ya ndani ya Halmashauri yatakayowezesha kuboresha huduma na kuanzisha miradi ya maendeleo .
Diwani mstaafu wa kata ya Kakukuru mzee Malima Mgeni ameuomba uongozi kuweka mkazo juu ya kuwepo kwa vikao vya wazee na kutengeneza heshima kwa wazee ili kuendelea kurithisha historia ya nchi na kuleta maadili mema.
Mbali na hayo Mhe.Ngubiagai amekemea vikali matukio ya uvamizi na uvunjifu wa amani yanayoendelea kuripotiwa ndani ya kata hiyo na kuwataka wananchi kuacha mara moja tabia hizo wakikaidi sheria itachukua mkondo wake.
Akihitimisha mkutano huo Mwenyekiti wa kijiji cha Mulutilima ndugu Isaya Nyembe Nyigino ameungana na wananchi wa Kakukuru kuishi kwa amani na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za uzalishaji kuleta maendeleo ndani ya kata hiyo.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.