Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe leo limefanya kikao cha Baraza Maalumu la kujadili Bajeti ya mwaka wa Fedha 2021/2022. Kikao hiko kimefanyika katika Ukumbi Mkubwa wa Halmashauri.
Akiwasilisha taarifa ya bajeti hiyo Mchumi wa Halmashauri Bw. Joachim Tungilo ametaja vipaumbele katika bajeti hiyo ikiwa ni kuimarisha miundombinu ya utoaji huduma za jamii, kiuchumi na kuimarisha miundombinu na mazingira ya utendaji kazi.
Kwa mwaka wa Fedha 2021/2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe inategemea kukusanya na kutumia kiasi cha Tsh. 37,108,335,271.00 ambapo Fedha hizo ni matumizi ya kawaida kutoka ruzuku ya Serikali kuu na mapato ya ndani, mishahara, Fedha za utekelezaji wa miradi ya Maendeleo.
Bi. Ester A. Chaula Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ameeleza kuwa Makisio ya Mapato ya ndani kwa mwaka wa Fedha 2021/2022 ni Tsh Bil 3.2 na kati ya hizo fedha zitakazoelekezwa kwenye miradi ni Tsh 1,058,575,226. “hivyo ni matumaini yetu kuwa huduma na miradi itakayotekelezwa itaenda kumnufaisha Mwananchi moja kwa moja” alisema Chaula.
Kupitia Baraza la Maalumu la Madiwani linaloongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Joshua Manumbu limepitisha kiasi hiko kwa matumizi ya mwaka wa Fedha 2021/22.
Manumbu amesema baraza limejipanga kuhakikisha mapato ya ndani yanakusanywa na kutumiwa vema na kiasi tengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo kitapelekwa kwani wananchi wanahitaji kuona mafanikio kupitia bajeti hii. “matarajio yetu ni kukusanya mapato na kuvuka lengo, hivyo kila mtendaji asimame imara katika majukumu yake” alisisitiza Manumbu.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.