Baraza la Madiwani linaloongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe George Nyamaha Diwani wa Kata ya Kagunguli (CCM) na Makamu Mwenyekiti Gabriel Kalala Gregory Diwani wa Kata ya Bukindo (CCM) wamekabidhi hundi kwa vikundi 24 vilivyoomba mikopo hiyo kwa shughuli mbali mbali za kiuchumi, jumla ya thamani ya hundi hizo ni Tsh 71,000,000/= .
Nyamaha amewapongeza vikundi hivyo kwa kupata mikopo hiyo na amewataka kutumia vema na kurudisha kwa wakati ili wengine waweze kukopeshwa kama wao walivyopata. Ni dhamira yetu kuhakikisha wananchi wa Ukerewe wanaweza kufanya na kujishughulisha katika kujiingizia kipato.
Innocent Gitubabu Maduhu Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ukerewe amesema fedha hizo zimetolewa kwa lengo la kuwainua kiuchumi kwani vikundi vyote 24 vilivyoomba vinashughuli za kiuchumi na wanapaswa kurejesha kama walivyoelekezwa. Pia kuwajengea vijana, walemavu na wanawake uwezo wa kujitegemea. “Ugawaji wa mikopo hii ni kutekeleza sera ya serikali ya kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ili kukopesha wanawake, vijana na walemavu”. Alisema Maduhu.
Cecilia Oswago Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 jumla ya mikopo yenye thamani ya Tsh. 51,744,000/= na ilitolewa kwa vikundi 13 vya wanawake, 4 vijana na 3 walemavu vikiwa na jumla ya wanufaika 307. Kuanzia mwaka wa fedha 2019/2020 hadi kufikia disemba 2019 jumla ya mkopo wa Tsh. 32,950,000/= umetolewa ambapo vikundi 9 vya wanawake wamekabidhiwa Tsh. 24,250,000/=, kikundi 1 cha vijana Tsh 5,700,000/= na kikundi kimoja cha walemavu Tsh 3,000,000/=.
Zoezi la ugawaji wa fedha hizo limefanyika katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri ambapo palitanguliwa na kikao cha Baraza hilo ambao waheshimiwa madiwani wamejadili taarifa za robo ya pili yani septemba hadi disemba.
Aidha Maduhu amelieleza baraza la madiwani kuwa Wilaya ya Ukerewe inategemea kupokea boti ya wagonjwa wa dharura ambapo majaribio ya boti hiyo yameshafanyika na boti inatarajiwa kufika wilayani Ukerewe hivi karibuni. Boti ya wagonjwa wa dharura (ambulance boat) itakuwa inabeba wagonjwa kutoka visiwani kupelekwa Hospitali ya Wilaya Ukerewe na Mwanza kwa matibabu yakibingwa.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.