Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kupitia divisheni ya afya,ustawi wa jamii na lishe, kitengo cha chanjo inaendelea na maboresho ya utoaji wa huduma za chanjo katika kuhakikisha kuwa jamii ya Ukerewe inapata huduma hiyo kwa vipindi stahiki kwa ubora.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo mratibu wa chanjo Wilaya ya Ukerewe Ndugu Rajab Abuu Hamza amesema jumla ya watoa huduma 66 kutoka vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya wamepatiwa mafunzo kuhusu mkakati wa vipindi maalum vya kuimarisha huduma za chanjo (PIRI) ambapo miongoni mwao wachanjaji ni 44 na wahudumu wa afya ngazi ya jamii 22.
Rajab amesema lengo la mafunzo hayo ni kujenga uelewa wa pamoja pia ni maandalizi ya zoezi la utoaji chanjo linalotarajiwa kuanza Novemba 29 hadi 03 Desemba 2025 .
Nae kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt.Revocutus Cleophace amewasihi wahudumu hao kuhakikisha wanawafikia watoto wote ambao hawajapata chanjo na wale ambao hawajakamilisha ratiba zao za chanjo sambamba na kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo katika kuwalinda watoto dhidi ya magonjwa yanayoweza kudhibitiwa na chanjo.
Chanjo zitakazotolewa ni chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano,surua lubela(MR), polio (sindano na matone), saratani ya shingo ya kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 9 na kuwafikia wasichana wenye umri wa miaka 10 hadi 14 ambao hawakufikiwa kwa wakati na chanjo zingine za kawaida.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.