Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amefanya ziara ya siku moja katika vijiji vya Malelema kata ya Bukungu kisiwani Ukara na Musozi kata ya Bukindo Wilayani Ukerewe. Lengo ikiwa ni kusikiliza changamoto za kiuchumi zinazowakumba katika sekta hizo vijijini humo.
Akizungumza kwenye mkutano huo Mhe. Ulega alianza kwa kutoa pole kwa wananchi wa Wilaya ya Ukerewe hasa wa kisiwa cha Ukara kutokana na ajali ya MV Nyerere iliyotokea tarehe 20 mwezi Septemba 2018, ikitimiza mwaka mmoja tangu kutokea kwa ajali hiyo. Pia alitoa pongezi kwa Wananchi kwa kuwa na Viongozi wazuri akitolea mfano Mhe. Pius Msekwa, aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile amewapongeza Wananchi wa kijiji cha Malelema kisiwa cha Ukara kwa kuwa mstari wa mbele kupinga Uvuvi haramu.
Wakielezea baadhi ya changamoto kubwa katika sekta ya uvuvi wananchi wa kijiji cha Malelema wanakabiliwa na sintofahamu kuhusu mipaka ya ziwa Victoria baina ya Tanzania na Uganda ikiwa ndo ziwa pekee linalotumika katika shughuli ya Uvuvi. Vilevile wameeleza mkanganyiko juu ya Zana sahihi zinazofaa kwa ajili ya Uvuvi.
Akijibu hoja ya Zana sahihi za Uvuvi, Afisa Uvuvi Wilaya ya Ukerewe ndugu Abbubakar Murshid amesema ndoano namba 1, 2, na 3, zinaruhusiwa kutumia kwa ajili ya shughuli za Uvuvi, namba 4, 5, 6, na 7 haziruhusiwi kabisa, pia namba 9, 10, 11, 12 na kuendelea zinaruhusiwa maeneo tengefu.
Mhe. Ulega akijibu hoja za wananchi amesema, suala la kuhusu mipaka Wizara italifanyia kazi, pia ametoa agizo la mwezi mmoja kwa wananchi kuunda vyama Ushirika ili kuweza kurahisisha upatikanaji wa mikopo kutoka Taasisi za kifedha, kama vile Benki na Vikundi mbalimbali. Aidha amezungumzia bado utafiti unafanyika kuhusu matumizi ya nishati ya juu (solar) katika shughuli ya uvuvi hivyo wavuvi waendelee kutumia taa za mafuta.
Halikadhalika ametoa agizo josho la mifugo katika kijiji cha Musozi kufanyiwa marekebisho na kuahidi kiasi cha shilingi milioni mbili (2,000,000) kama kianzio cha marekebisho hayo. Pia amesisitiza kushughulikia suala la kuongeza wataalamu wa mifugo ili wananchi kuweza kupata huduma staiki. Vilevile amepokea ombi la mfumo wa ukopeshaji wa mifugo uliojulikana kama “kopa ng’ombe lipa ngo’mbe” uliokuwepo hapo awali.
Akihitimisha mkutano katika kijiji cha Malelema kisiwani Ukara, Mhe. Cornell Magembe Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, amesisitiza wananchi kuhudhuria vikao mbalimbali vinavyo itishwa na viongozi wa serikali kwa ajili ya maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.