Kisiwa cha Gana ni moja ya visiwa vinavyounda Wilaya ya Ukerewe ambapo shughuli kuu za kiuchumi katika Wilaya ya Ukerewe na visiwa vyake ni Uvuvi kwa kiwango kikubwa na kilimo, hivyo wavuvi wametakiwa kujihusisha na uvuvi unaofuata sheria, kanuni na taratibu kwani utasaidia kuongeza kipato cha wavuvi na pato la serikali kiujumla.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ukerewe Frank S. Bahati amefanya ukaguzi wa mialo katika kisiwa cha Gana na kujionea shughuli mbali mbali za uvuvi wa samaki na dagaa, ambapo alitembelea kukagua maeneo ya uvuvi na shughuli wanazifanya katika maeneo ya mialo.
Katika ziara hiyo Bahati aliambatana na Afisa Uvuvi wa Wilaya Abubakari Murshid ambapo walikagua vipimo au rula ya kupima samaki waliokidhi vigezo vya kuvuliwa, hivyo akawaagiza wavuvi wote wa samaki wanatakiwa kuwa na rula yenye vipimo sahihi ambazo hazipotoshi na mizani ziwe nzima. Na kwa yeyeto atakaye bainika kwenda kinyume na maelekezo atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Katika shughuli nyingine Bahati ameongoza idara ya Uvuvi na mifugo katika uchomaji wa zana za uvuvi haramu zilizokamatwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya na kutoa tamko kuwa patakua na kikosi kazi cha wataalamu wa uvuvi na doria za uvuvi watakao kuwa wakiishi katika visiwa ili kuweza kuangalia kwa ukaribu shughuli za uvuvi ili kukabiliana na uvuvi haramu unaofanywa na watu wachache wasio penda kufuata na kutii sheria, kanuni na taratibu.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.