".. Wananchi mjitokeze kwa wingi kuja kuona na kujifunza maboresho yenye ubunifu mkubwa katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi.."
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe.Hashim Abdalah Komba aliemwakilisha mgeni rasmi Mkuu wa mkoa wa Geita wakati alipokuwa akifungua maonesho ya wakulima nane nane katika viwanja vya Nyamhongolo vilivyopo wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Akisoma taarifa ya maonesho hayo Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mwanza Ndg. Peter Kasele amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la washiriki kila mwaka hali inayoonyesha utayari wa watu katika kujifunza na kupokea vitu vipya.
Aidha Mhe.Komba amewataka wananchi kujifunza kilimo cha eneo dogo chenye tija huku akiwasihi kujipanga na kuchukua mikopo yenye tija kutoka taasisi mbalimbali za kifedha zinazoshiriki ili kukuza vipato vyao katika shughuli wanazojighulisha nazo .
Nae mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Mwanza ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde.Christopher E.Ngubiagai amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha na kuendelea kuwekeza katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi ikiwa sehemu ya kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.
Mbali na hayo Mhe.Komba amegusia kauli mbiu ya maonesho hayo isemayo Chagua viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi 2025 kwa kutoa Rai kwa wananchi kujiandaa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29 ,2025 huku akitaja sifa za kiongozi bora kuwa ni kuja na ubunifu mkubwa wa kugusa maisha ya watu wengi.
Julia Masatu ni miongoni mwa washiriki kutoka wilaya ya Ukerewe yeye anapongeza serikali kwa kuwapa fursa hiyo kufanya biashara huku akiomba fursa za namna hiyo kuongezeka zaidi katika maeneo yao.
Maonesho ya wakulima nane nane kanda ya ziwa magharibi yanahusisha mikoa miwili ya Mwanza na Geita kuanzia Agosti 1 hadi Agosti 8 2025 .
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.