".. tuondokane na fikra za zamani na mazoea juu ya uwekezaji katika eneo la uvuvi tu tuitumie ardhi pia, tulifanye zao la kahawa kuwa nguzo ya pili ya uchumi wetu. Serikali imeweka nguvu kubwa katika zao hili ili kuongeza ajira kwa vijana na kipato kwa wananchi wa Ukerewe .."
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cde, Christopher Ngubiagai katika hafla ya ugawaji wa miche ya zao la kahawa katika kijiji cha Busagami kata ya Namilembe ambapo jumla ya miche 26,000 imegawiwa kwa vyama vya ushirika (AMCOS) 14 vilivyopo wilayani Ukerewe.
Aidha Cde, Ngubiagai amesema maendeleo ya kweli hayaji kwa maneno bali kwa vitendo, amewataka wananchi kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilimo kwa kulienzi zao hilo na kulisimamia ili kukuza uchumi huku akiweka wazi ujio wa miche mingine zaidi ya laki nne katika wilaya ya Ukerewe.
Nae Mwenyekiti wa Nyanza Cooperative Union (NCU) ndugu Leonard Lyabalima amesema kahawa ina uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha ya wanaukerewe nakuiomba serikali kuwapa kipaumbele wakulima wa zao hilo na kuahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa wakulima.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe ndugu Wanchoke Chinchibela amesema Halmashauri itakuwa bega kwa bega na wakulima wote na kuwaagiza maafisa ugani kuendelea kusimamia na kutoa elimu juu ya ustawi wa miche hiyo.
Mkufunzi na mzalishaji wa kahawa Bi. Amina Yusuph Kashoro amewataka wakulima kulinda miche yao kwa kuzingatia mahitaji yote kama mbolea na kumwagilizia maji kwa vipindi na kuwa waangalifu wa mifugo ili kufaidi matunda ya kilimo cha zao hilo.
Ernest Andrew Goroba ni mwanachama wa AMCOS Nduruma yeye amepongeza jitihada za serikali kurejesha zao hilo lililowanufaisha zamani huku akiwaomba wana ukerewe kulipokea kwa mikono miwili ili kuijenga kesho bora ya Ukerewe.
Cde, Ngubiagai amehitimisha hafla hiyo kwa kutoa rai kwa wana ukerewe wote kuijenga Ukerewe ya kijani kupitia zao la kahawa na kuahidi ushirikiano wa moja kwa moja kwa wakulima wote ili kujenga mazingira rafiki ya kilimo cha biashara wilayani humo.
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.