Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbai Wilaya ya Ukerewe na visiwani ambapo ametembelea kisiwa cha Ukara. Hii ni miradi iliyotembelewa na Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella na maelekezo aliyoyatoa katika miradi hiyo.
Kijiji cha Busunda kiko kata ya Bukanda, tarafa ya Mumbuga. Kijiji hiki kilianza kutekeleza mradi huu mwaka 2014 kwa nguvu za wananchi. Mwaka wa fedha 2016/17 Halmashauri imepeleka fedha za Miradi kupitia Ruzuku ya Maendeleo - CDG ili kukamilisha ujenzi wa zahanati ukisimamiwa na Kamati ya Maendeleo ya Kata - WDC kwa kushirikiana na wananchi. Lengo la mradi huu ni kutoa huduma za afya kwa wakazi wanaoishi kijiji cha Busunda wanaokadiriwa kuwa wakazi 3,225.
Mradi wa ukamilishaji wa ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Busunda umekamilika kubakiwa namawe trip 6, mchanga trip 3, kokoto trip 1 na tofali 430. Mradi huu umegharimu kiasi cha Tsh. 26,800,000.00. Michango ya Jamii Tshs. 6,800,000.00 imetumika kunyanyua jengo hadi usawa wa renta. Ruzuku toka serikalini (CDG) Tshs. 20,000,000.00 iliyotumika kununulia vifaa kwa ajili ya kukamilisha mradi. Kata na Halmashauri zimejipanga na kuanzisha ujenzi wa nyumba ya mganga kwa kuhamasisha wananchi kuchangia ujenzi huo ili serikali iweze kukamilisha na hatimaye mradi kutoa huduma iliyokusudiwa.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella amepongeza ujenzi mzuri wa Zahanati ya Busunda na kuitaka idara ya ujenzi kufanya ufuatiliaji wa viwango vya majengo na kufanya marekebisho kulingana na vigezo vya ujenzi wa majengo ya serikali.
Ukamilishaji Ujenzi wa Nyumba ya Mganga Kituo cha Afya Kagunguli.
Mradi wa ujenzi wa nyumba ya mganga ulianza kutekelezwa mwaka 2013/14 kwa fedha toka Serikalini kupitia Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM). Mwaka 2016/17 Halmashauri imepokea fedha za Miradi ya Maendeleo - CDG ambazo zimetegwa kukamilisha mradi huu. Lengo la mradi huu ni kuhakikisha waganga wanapata mazingira mazuri ya kuishi ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa haraka pale wanapokuwa wanahitajika. Mradi wa ujenzi wa nyumba ya mganga umetekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ulitekelezwa hadi hatua ya kuezeka jengo. Kwa sasa utekelezaji unaofanyika ni uwekaji wa vigae, mageti ya mlango na milango, ukamilishaji wa vyoo na upakaji wa rangi. Mradi huu unategemewa kugharimu jumla ya Tshs. 40,000,000.00.
Ujenzi wa Nyumba ya Watumishi (Two in One) Kata ya Bwisya.
Mradi wa ujenzi wa nyumba ya watumishi (two in one) ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2011/12 chini ya usimamizi wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Bwisya - WDC kwa fedha za ruzuku ya Maendeleo - CDG. Lengo la mradi huu ni kuhakikisha watumishi (Mtendaji wa Kata na Afisa Tarafa) wanapata mazingira mazuri ya kuishi ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi na haraka pale wanapokuwa wanahitajika. Mradi huu upo hatua ya ujenzi wa ukuta. Mradi unakabiliwa na changomoto ya ukosefu wa nguvu ya wananchi kipindi cha utekelezaji. Jumla ya Tshs. 17,000,000.00 zilitolewa kutoka ruzuku ya serikali - CDG ili kuunga mkono nguvu za wananchi. Fedha zote zilitumika bila kuwa na nguvu ya wananchi vifaa vilivyopo ni pamoja na mabati, misumari, mbao kwa ajili ya milango na nondo.
Katika mradi huu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella alibaini kuwepo kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha zilizotumika katika ujenzi wa nyumba hiyo ambapo aliagiza OCD kumkamata Diwani wa kata hiyo Mhe. Dismas Busanya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mtendaji wa kata alikuwepo kipindi mradi unatekelezwa ndugu Ladslaus Mabagala ambaye sasa anahudumu kama Mtendaji wa kata ya Bukanda.
Skimu ya Umwagiliaji ya Miyogwezi.
Skimu ya umwagiliaji ya Miyogwezi ipo katika bonde la Miyogwezi ambalo limezungukwa na vijiji vya Igongo, Kameya, Muriti na Busagami. Eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji katika bonde hili ni Ha. 120. Mpaka sasa eneo lililoendelezwa na kujengwa miundombinu ya umwagiliaji ni Ha. 40 tu, na chanzo kikuu cha maji ni mto Miyogwezi. Wanufaika wa moja kwa moja wa mradi huu ni wakulima 194 (me 143, ke 51) wanaomiliki maeneo katika bonde hili. Mazao makuu yanayolimwa katika skimu hii ni Mpunga, Viazi vitamu na mazao ya bustani.
Mradi wa Miyogwezi ulianza kujengwa tarehe 01/05/2013 hadi tarehe 07/10/2013 kwa hatua ulipofikia. Kazi ya kutangaza zabuni ya ujenzi wa mradi huo ilifanyika ngazi ya Wizara ya Kilimo na Kampuni iliyoshinda zabuni ya kujenga mradi huo ni “Comfix & Engineering Ltd” ya Dar es Salaam ambayo ilitambulishwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe na Ofisi ya Mratibu wa mradi wa DASIP kitaifa – Mwanza.
Ujenzi wa mradi wa Miyogwezi ulikuwa ukisimamiwa na mamlaka zifuatazo:
DASIP makao makuu Mwanza walikuwa wasimamizi wa masuala ya utawala na fedha katika ujenzi wa mradi huu. Kampuni ya CODA ya Kenya ilikuwa ni mtaalam mshauri (Consultant) wa mradi ambaye alipatikana ngazi ya wizara. Kampuni hii ndiyo ilikuwa inasimamia kazi zote za kitaalamu, kuthibitisha ubora wa kazi na kuandaa hati za malipo kwa kila hatua iliyokuwa ikikamilika.
Ofisi ya umwagiliaji kanda ilikabidhiwa kusimamia miradi yote iliyokuwa chini ya DASIP na ambayo ilikuwa haijakamilika baada ya mradi wa DASIP kufikia mwisho wa utekelezaji tarehe 31 Desemba 2013.
Kazi zilizofanyika katika ujenzi wa skimu Ujenzi wa mabanio 2 (Headworks) na mageti, Ujenzi wa mifereji mikuu 2, Mfereji Na 1, una urefu wa mita 1,425 ambapo mita 560 zimejengwa kwa mawe na sementi na mita 865 hazikujengewa. Mfereji Na 2, una urefu wa mita 1,725. Kati ya hizo mita 535 zimejengwa kwa mawe na sementi na mita 1,190 hazikujengewa. Ujenzi wa vigawa maji 6 (diversion boxes) katika mfereji Na.1 na vigawa maji katika mfereji Na 2. Ujenzi wa kalvati 1 katika mfereji Na 1 na kalvati 2 katika mfereji Na 2.
Fedha iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi ilikuwa ni Tshs 771,797,110/=, kiasi kilicholipwa ni Tshs 684,050,713/= na kiasi cha fedha Tshs 76, 005, 634.86 zilikuwa hazijalipwa kwa mujibu wa maelezo ya barua ya Mratibu wa mradi wa DASIP kitaifa.
Changamoto ni ukosefu wa fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi, Muda wa utekelezaji wa mradi wa DASIP kuisha mapema kabla ya mradi wa umwagiliaji kukamilika. Mkandarasi kupatikana ngazi ya Taifa na mkataba wa ujenzi kufungwa ngazi ya Wizara. Jitihada zilizo kwisha fanywa na wilaya tangu kusimama kwa mradi, Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na Mkoa pamoja na Ofisi ya Umwagiliaji Kanda tumeendelea kuomba fedha Wizarani kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi. Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji (W) na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya zimekuwa zikiendelea kufuatilia mkakati wa ukamilishaji wa mradi huu toka Ofisi ya Umwagilaji Kanda.
Ujenzi wa Mradi wa Maji Kazirankanda.
Ujenzi wa mradi wa maji Kazirankanda unaohusisha vijiji 13, ulianza mwaka 2013 na unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Disemba 2017. Kazi za ujenzi wa mradi zinatekelezwa na wakandarasi watano ambao ni Pet Coop LTD anayejenga mfumo wa kuvuta maji toka ziwani na kusukuma kwenye tanki la Lutare na kusambaza maji katika kijiji cha Lutare, Make Engineering Ltd anayejenga Mfumo wa maji kwenye vijiji vya Buhima na Igalla, Cyril Investiment anayejenga katika vijiji vya Kigara na Bwasa, Ndeenengo Senguo Co Ltd anayejenga katika vijiji vya Muhula, Mahande, Namasabo na Busunga, D4N anayejenga katika vijiji vya Namagondo,Kazirankanda na Hamuyebe, na Chiland CO LTD anayejenga katika kijiji cha Malegea. Mradi huu unagharimu kiasi cha Tsh 6,968,516,977 na mpaka sasa kiasi cha Tsh 5,114,118,511 kimelipwa sawa na asilimia 73 na zaidi ya asilimia 85 ya kazi imefanyika mpaka sasa.
Mpaka kukamilika kwa mradi takribani wakazi 68,000 watanufaika na mradi huu hivyo kupelekea asilimia ya wakazi wanaopata maji safi na salama katika wilaya ya Ukerewe kufikia 265,763 sawa na asilimia 77. Hali kadhalika ,upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya mradi utapelekea kupungua kwa magonjwa kama vile kipindupindu na kuogeza muda kwa ajili ya kufanya shughughuli za kimaendeleo kama vile klimo na uvuvi. Fedha zitakazopatika kutokana na makusanyo ya maji zitasaidia kuongeza vituo vingine zaidi vya kuchotea maji hasa kwenye maeneo yaliyokosa vituo hivyo.
Mradi huu utakapokamilika utakabithiwa katika vijiji husika ambavyo tayari vimeunda vikundi vya watumia maji (COWSO). Vikundi hivi vimejengewa uwezo juu ya utunzaji, usimamizi, ulinzi na ukusanyaji wa mapato ya maji. Uongozi Halmashauri pamoja na COWSO kwa kushirikiana na vijiji husika vitajadili na kupanga utaratibu mzuri wa kuendesha mradi huu kwa ufanisi ili kuhakikisha mradi unakuwa endelevu na wenye manufaa.
Ujenzi wa Hostel katika Shule ya Sekondari Bwisya.
Shule ya sekondari Bwisya ilianzishwa mwaka 1992 ikiwa chini ya Bodi ya wakulima. Mwaka 1994 Bodi ya wakulima iliikabidhi shule hii Serikalini. Mradi wa ujenzi wa Hosteli ya Shule ya Sekondari Bwisya ulitekelezwa mwaka wa fedha 2014/15 kwa kutumia fedha ya Ruzuku ya Maendeleo toka Serikali kuu. Mradi huu unalenga kuboresha mazingira ya kujifunza kwa kupunguza umbali wa wananafunzi kufika shuleni ili kuongeza ufaulu na hivyo kuinua kiwango cha taaluma. Mradi wa ujenzi wa hosteli umeshakamilika ambapo utakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 96. Jumla ya Tshs 200,000,000 ilitolewa na Serikali kuu ikiwa ni Ruzuku ya Maendeleo. Kiasi cha Tshs. 199,848,000 kilitumika katika ujenzi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella ameagiza shule ya sekondari Bwisya maombi yapelekwe serikalini na kuanza kutumika kama shule ya bweni iliserikali iwe inapeleka fedha za kugharamia wanafunzi watakaokuwa wakiishi shuleni hapo na amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuhakikisha kuwa shule itakapofunguliwa mabweni hayo yaanze kutumika mara moja.
Ujenzi wa Choo cha Wanafunzi Shule ya Msingi Muhozya.
Shule ya Msingi Muhozya iko kijiji cha Bulamba, kata ya Bukindo. Shule hii ina wanafunzi 738 (wavulana 369 na wasichana 369) Mradi wa ujenzi wa choo ulianza mwezi Machi 2017 kwa nguvu za wananchi na fedha za ruzuku ya maendeleo - CDG. Lengo la mradi huu ni kuboresha mazingira ya kujifunza na kujifunzia kwa wanafunzi ili kuboresha kiwango cha elimu.
Ujenzi wa shimo la choo cha wanafunzi limekamilika na ujenzi wa vyumba 12 vya choo uko katika hatua ya renta na ujenzi unaendelea. Jumla ya Tshs. 5,000,000.00 zilitolewa kusaidia nguvu za wananchi kukamilisha ujenzi wa choo. Mchango wa wananchi katika kutekeleza mradi huu ni tofari 7,000 za kuchoma, kokoto, mchanga na maji. Halmashauri inaendelea na mkakati wa uhamasishaji wa jamii kuendelea kuchangia nguvu ili kukamilisha mradi huu.
Ujenzi wa Choo cha Wanafunzi Shule ya Msingi Mukasika.
Shule ya Msingi Mukasika iko kijiji cha Mukasika, kata ya Namagondo. Shule hii ina jumla ya wanafunzi 618 (Wavulana 301na Wasichana 317) na walimu 10. Mradi wa ujenzi wa choo ulianza mwezi Machi 2017 kwa nguvu za wananchi kwa fedha za Malipo kwa Ufanisi (P4R).
Lengo la mradi huu ni kuboresha mazingira ya kujifunza na kujifunzia kwa wanafunzi ili kuboresha kiwango cha elimu. Mradi wa ujenzi wa choo cha wanafunzi unatekelezwa kwa kujenga matundu 9 ya vyoo ambapo jengo limeezekwa na ujenzi unaendelea. Jumla ya Tshs. 3,000,000.00 zilitolewa kusaidia nguvu za wananchi kukamilisha ujenzi wa choo. Mchango wa wananchi katika kutekeleza mradi huu ni tofari, kokoto, mchanga na maji. Halmashauri inaendelea na mkakati wa uhamasishaji wa jamii kuendelea kuchangia nguvu ili kukamilisha mradi huu.
Utengenezaji wa Madawati katika Kituo cha Ufundi Bukongo.
Serikali ilitoa agizo la utengenezaji wa madawati kwa wilaya zote nchini ili kutatua tatizo la uhaba wa madawati katika shule zote za msingi na sekondari. Wilaya ya Ukerewe iliitikia agizo hili la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutengeneza madawati kupitia kituo cha Ufundi kilichoko shule ya Msingi Bukongo na Jitihada za serikali kuu, taasisi za serikali ambazo ni Wakala wa Misitu - TFS, Shirika la umeme - TANESCO na Rubya Forest. JKT Mugulani, Taasisi za Fedha -NMB, makapuni ya simu Tigo, Wananchi, Wafanyabiashara na wadau mbalimbali waliowezesha upatikanaji wa madawati.
Utekelezaji wa agizo hili ulianza mwaka 2015 ambapo Wilaya ilikuwa na wanafunzi 102,114 ambao walihitaji madawati 34,038. Madawati yaliyokuwepo ni 16,413 hivyo kuwa na upungufu wa madawati 17625. Jumla ya madawati 11,489 yametengenezwa na kugawika katika shule mbalimbali za msingi. Hivyo kuwa na upungufu wa madawti 6,136.
Aidha Wilaya imepokea madawati 400 toka wakala wa misitu Tanzania - TFS yatakayogawika kwa shule 20. Wilaya imegawa mbao 150 shule Msingi Bukongo kwa ajili ya kutengeneza madawati 65 na mbao 12,689 kwa shule 59 ambazo zinategemewa kutengeneza madawti 4,229. Hivyo, upungufu ni madawati 1,442.
Kutokana na takwimu za uandikishaji wa darasa la Awali na darasa la kwanza mwaka huu 2017 idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka wanafunzi 102,114 mwaka 2016 hadi 107,481 Machi 2017 sawa na ongezeko la wanafunzi 5,367 wanaohitaji madawati 1,789. Kutokana na takwimu hizi mpaka sasa wilaya ina upungufu wa madawati 3,231 ambao unaendelea kushughulikiwa.
Kituo cha Afya Bwisya.
Kituo cha afya Bwisya kilifungulia mwaka 1978 kwa lengo la kuwasogezea huduma wananchi wa kisiwa cha Ukara. Kituo hiki kina jumla ya watumishi 11 na kinahudumia wakazi wapatao 37,704,804 wanakadiriwa kuishi katika kisiwa cha ukara kwa mujibu wa Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2012.
Tangu kuanzishwa kwa kituo hiki Halmashauri imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuendeleza kituo hiki ili kiweze kutoa huduma bora kwa wananchi wa kisiwa cha Ukara. Jitihada ambazo zimekuwa zikifanyika ni pamoja na Ujenzi wa nyumba za watumishi ambapo mpaka sasa jumla ya nyumba kumi na tano za watumishi zimekwishajengwa. Ujenzi wa wodi 2 za wagonjwa, jengo la upasuaji, jengo la kutolea huduma ya mama na mtoto (RCH), pamoja na jengo dogo la kutolea huduma kwa wagonjwa wa nje na huduma ya kujifungulia mama wajawazito. Kuandaa mpango wa kituo (Master Plan) ambayo itatumika katika utekelezaji wa uendelezaji wa miundo mbinu ya kituo. Ukarabati wa majengo ya kituo kupita mpango wa malipo kwa ufanisi - RBF.
Aidha katika mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya Tsh 80,000,000/= zimetengwa kwa ajili ya ukamilishaji wa nyumba moja ya mtumishi, ukarabati wa miundo mbinu ya jengo la upasuaji pamoja na ukarabati wa mfumo wa umeme kituoni. Hata hivyo katika mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya Tsh 504,151,451/= zimetengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za mishara, matumizi ya kawaida na Miradi ya maendeleo ili kuhakikisha kituo hiki kinatoa huduma stahiki wa wakazi wa Ukara. Pia tunaishukuru serikali kwa kukubali mapendekezo yetu na kukichagua kituo cha Afya Bwisya kuwa miongoni mwa vituo mia moja ambavyo vitapewa msaada kwa ajili ya uboreshaji wa miundo mbinu ya kutolea huduma za afya. Serikali imeletea Tsh. 10,000,000/= kutoka mpango wa RBF na imekuwa na mafanikio makubwa katika kukarabati majengo ya kituo hiki kwa lengo la kuboresha huduma za afya zitolewazo.
Zahanati ya Hamuyebe.
Zahanati ya Hamuyebe ipo kijiji cha Hamuyebe kata ya Bukanda Wilaya ya Ukerewe. Zahanati hii ilifunguliwa mwaka 2014 na inahudumia wakazi wa kijiji cha Hamuyebe, Namasabo na baadhi ya wakazi toka kata ya Nakatunguru. Huduma za wagonjwa wa nje, huduma za Afya ya baba, mama na mtoto, huduma za kujifungua, huduma za uzazi wa mpango, huduma za ushauri nasaha na ipimaji wa VVU. Zahanati ilipokea fedha za Malipo kwa ufanisi - RBF kiasi cha Tsh. 10,000,000/= mnamo mwezi wa Agasti 2016 kwa ajili ya ukarabati wa zahanati na ununuzi wa vifaa tiba. Shughuli hii ilifanyika chini ya kamati ya usimamizi wa huduma za zahanati.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella katika zahanati hii amewataka idara ya Ujenzi na kata kuongeza ukubwa cha chumba cha kujifungulia na kiwekewe vifaa vya kupunguza sauti na madirisha imara.
Ujenzi wa Mradi wa Maji Bukindo.
Ujenzi wa mradi wa maji Bukindo ulianza mwezi Machi 2017 na unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Septemba 2017. Kazi za ujenzi wa mradi zinatekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na maji taka Mwanza. Mradi huu unagharimu kiasi cha Tsh 150,000,000. Mpaka kukamilika kwa mradi ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita 300,000 kwa siku takribani wakazi 5000 wa maeneo ya Bukindo na Kagunguli watanufaika na mradi huu. Hata hivyo uongozi wa wilaya kwa kushiriana na MWAUWASA una mpango wa kuhakikisha maji kwa ajili ya mradi huu yanafika katika chuo cha Murutunguru, shule ya Pius Msekwa na taasisi zilizo karibu na maeneo hayo . Hali kadhalika ,upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya mradi utapelekea kupungua kwa magonjwa kama vile kipindupindu na kuongeza muda kwa ajili ya kufanya shughuli za kimaendeleo kama vile kilimo na uvuvi. Fedha zitakazopatika kutokana na makusanyo ya maji zitasaidia kuongeza vituo vingine zaidi vya kuchotea maji hasa kwenye maeneo yaliyokosa vituo hivyo.Kwa kuanza tutajenga vituo 10 vya kuchotea Bukindo na Kagunguli, Adha Mradi utakuwa na mfumo wa kutibu maji kwa kutumia dawa ya caicium hypochlorite.
Mradi huu utakapokamilika utakabidhiwa katika vijiji husika ambavyo vitaweka utaratibu wa kuunda Kamati ya watumiaji maji. Vikundi hivi vitajengewa uwezo juu ya utunzaji,usimamizi ,ulinzi na ukusanyaji wa mapato ya maji.Uongozi wa Halmashauri pamoja na COWSO kwa kushirikiana na vijiji husika vitajadili na kupanga utaratibu mzuri wa kuendesha mradi huu kwa ufanisi ili kuhakikisha mradi unakuwa endelevu na wenye manufaa. Mradi huu umechukua muda mrefu kukamilika hali iliyosababishwa na upungufu wa fedha. Hata hivyo Mamlaka ya maji safi na maji taka Mwanza inafanya juhudi za kutafuta fedha kwa kushirikiana na wizara ya maji ili kukamilisha mradi huu.Ufuatiliaji unafanyika ili kuhakikisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu zinapatikana mapema.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.